Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™
Isaya 12
1Katika siku ile utasema: “Nitakusifu wewe, Ee Bwana . Ingawa ulinikasirikia, hasira yako imegeukia mbali nawe umenifariji.
2Hakika Mungu ni wokovu wangu; nitamtumaini wala sitaogopa. Bwana , Bwana , ni nguvu zangu na wimbo wangu; amekuwa wokovu wangu.”
3Kwa furaha mtachota maji kutoka visima vya wokovu.
4Katika siku hiyo mtasema: “Mshukuruni Bwana , mliitie jina lake; julisheni miongoni mwa mataifa yale aliyoyafanya, tangazeni kuwa jina lake limetukuka.
5Mwimbieni Bwana , kwa kuwa ametenda mambo makuu, hili na lijulikane duniani kote.
6Pazeni sauti mwimbe kwa furaha, watu wa Sayuni, kwa maana mkuu ni yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli miongoni mwenu.”