Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™
Zaburi 128
1Heri ni wale wote wamchao Bwana , waendao katika njia zake.
2Utakula matunda ya kazi yako; baraka na mafanikio vitakuwa vyako.
3Mke wako atakuwa kama mzabibu uzaao ndani ya nyumba yako; wana wako watakuwa kama machipukizi ya mizeituni kuizunguka meza yako.
4Hivyo ndivyo atakavyobarikiwa mtu amchaye Bwana .
5Bwana na akubariki kutoka Sayuni siku zote za maisha yako, na uone mafanikio ya Yerusalemu,
6nawe ujaliwe kuishi uone watoto wa watoto wako. Amani iwe juu ya Israeli.