KING JAMES BIBLETafuta

Biblica® Toleo Wazi Neno: Bibilia Takatifu™

Zaburi 86

Zote · ZaburiTafuta

1Ee Bwana , sikia na unijibu, kwa maana mimi ni maskini na mhitaji.

2Linda maisha yangu, kwa maana nimejiweka kwako, wewe ni Mungu wangu, mwokoe mtumishi wako anayekutumaini.

3Ee Bwana , nihurumie mimi, kwa maana ninakuita mchana kutwa.

4Mpe mtumishi wako furaha, kwa kuwa kwako wewe, Ee Bwana , ninainua nafsi yangu.

5Ee Bwana , wewe ni mwema na mwenye kusamehe, umejaa upendo kwa wote wakuitao.

6Ee Bwana , sikia maombi yangu, sikiliza kilio changu unihurumie.

7Katika siku ya shida yangu nitakuita, kwa maana wewe utanijibu.

8Ee Bwana , katikati ya miungu hakuna kama wewe, hakuna matendo ya kulinganishwa na yako.

9Ee Bwana , mataifa yote uliyoyafanya yatakuja na kuabudu mbele zako; wataliletea utukufu jina lako.

10Kwa maana wewe ni mkuu, na unafanya mambo ya ajabu; wewe peke yako ndiwe Mungu.

11Ee Bwana , nifundishe njia yako, nami nitakwenda katika kweli yako; nipe moyo usiositasita, ili niweze kulicha jina lako.

12Ee Bwana wangu, nitakusifu kwa moyo wote; nitaliadhimisha jina lako milele.

13Kwa maana upendo wako ni mkuu kwangu; umeniokoa kutoka kwenye vilindi vya kaburi.

14Ee Mungu, wenye majivuno wananishambulia; kundi la watu wakatili linatafuta uhai wangu: watu wasiokuheshimu wewe.

15Lakini wewe, Ee Bwana , ni Mungu wa huruma na neema, si mwepesi wa hasira, bali ni mwingi wa upendo na uaminifu.

16Nigeukie na unihurumie; mpe mtumishi wako nguvu zako, mwokoe mwana wa mtumishi wako wa kike.

17Nipe ishara ya wema wako, ili adui zangu waione nao waaibishwe, kwa kuwa wewe, Ee Bwana , umenisaidia na kunifariji.

Sources and attribution